COSOTA YASHIRIKI SHIRIKISHO LA KIMATAIFA LA KUSIMAMIA WATUNZI WA KAZI ZA SANAA
Tanzania kupitia COSOTA imeshiriki mkutano wa Shirikisho la Kimataifa la kusimamia watunzi wa kazi za sanaa (International Federation of Authors and Composers Societies - CISAC) ikiwa kama moja ya taasisi zinazosimamia masuala ya sanaa katika muziki na sanaa za ufundi.
Katika mkutano wa "CISAC Regional Committee (CAF)" uliofanyika tarehe 1 na 2 Juni 2026 masuala mbalimbali yamejadiliwa kuhusu maendeleo, fursa na changamoto katika masuala ya hakimiliki na Akili Unde (Artificial Intelligence), mifumo ya usajili na kuhakikisha usahihi katika usajili wa kazi; ukusanyaji na ugawaji mirabaha hasa katika mashirika ya utangazaji, mitandao na Tozo ya hakimiliki (Private Copy Levy); haki ya kupata kipato baada ya kazi kuuzwa katika mnada (resale right); uanachama wa taasisi zinazosimamia hakimiliki; umuhimu pamoja na mashirikiano ya taasisi za hakimiliki.
Aidha, katika mkutano huo, COSOTA kupitia Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Bi. Naomi Mungure, iliwasilisha maombi ya taasisi zilizoendelea kuweza kufanya kazi kwa karibu na Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha katika kazi za muziki ijulikanayo kama "Society of Music Advocacy" (SOMA) na Ofisi ya Hakimiliki Zanzibar (COSOZA) ili kuweza kukidhi vigezo vya kuwa wanachama wa taasisi hii, maombi ambayo yalikubaliwa. Aidha, COSOTA itasitisha kuwa mwanachama katika masuala ya muziki kutokana na kuwa sasa haikusanyi na kugawa mapato ya muziki. Ni matarajio kuwa CMO ya SOMA itajiunga rasmi na kuendeleza ushiriki wa Tanzania. Tanzania inawasilisha maombi rasmi ya kujiunga upande wa makusanyo ya mirabaha ya hakimiliki kupitia mauzo ya kazi za sanaa hasa katika minada (resale right) kwani Sheria na Kanuni imeshaweka mazingira tayari kwa ukusanyaji wa mapato haya kupitia COSOTA kutokana na kuwa bado hakuna CMO katika masuala ya sanaa za ufundi.
Sambamba na mkutano huu COSOTA imeweza kukutana na SACEM (CMO Ufaransa), GEMA (CMO Ujerumani), CAPASSO (CMO Afrika Kusini), SODAV (CMO Senegal), COSBOTS (CMO Botswana), SAMRO (CMO Afrika Kusini), MLC (CMO London) kwa lengo kuendeleza ushirikiano katika usimamizi wa hakimiliki Tanzania na inategemea kuonana na taasisi zinazosimamia resale right katika mikutano.
