Naibu Waziri Hamis Mwinjuma atoa agizo la kuchukuliwa hatua wadaiwa sugu wasiyolipa ya Leseni za matumizi ya muziki katika biashara
Naibu Waziri Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Hamis Mwinjuma ametoa agizo kwa Ofisi ya Hakimiliki kuwachukulia hatua watumiaji sugu wa kazi za sanaa kama Muziki na Filamu katika maeneo ya biashara ambao hawalipii leseni hizo (mirabaha).
Naibu Waziri Mwinjuma ametoa agizo hilo leo Machi 16, 2023 alipotembelea Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) baada ya kuapishwa kwake ikiwa ni ziara ya kufahamu majukumu ya taasisi zilizo chini ya Wizara.
"Ni lazima mfanye operesheni kwa hawa wadaiwa sugu ambao wanatumia kazi hizo lakini hawataki kulipa Mirabaha na kuwafanya mfano, Wasanii wameshateseka sana na sasa inatosha. Wao ni wakina nani hata watumie kazi za wasanii bila wasanii kunufaika" alisema Mhe. Mwinjuma.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya COSOTA Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Bibi.Doreen Anthony Sinare alieleza Ofisi inampango wa kugawa mirabaha hivi karibuni kabla ya kuanzishwa kwa makampuni ya ukusanyaji na Ugawaji wa Mirabaha.
"Tunafikiria Makampuni ya kukusanya na kugawa Mirabaha yatakapopewa leseni yaanze kazi tarehe 01.07.2023 ambapo itakuwa ni kipindi cha mwaka mpya wa fedha na COSOTA kwa wakati huo itakuwa tayari imefanya mgao," alisema Doreen.
Halikadhalika Naibu Waziri huyo alieleza kuwa amepewa jukumu la kusimamia Ofisi ya Hakimiliki na Mheshimiwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt.Pinda Chana kwa lengo la kuhakikisha masuala ya hakimiliki za Wasanii yanatekelezwa vyema.
Vile vile Mhe. Naibu Waziri Mwinjuma alipongeza COSOTA kwa kukamilisha mchakato wa utekelezaji wa mabadiliko ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya mwaka 2022 kwa wakati, ambapo alisisitiza kufanya kazi zaidi ili kutimiza adhima nzima ya kuboresha usimamizi wa hakimiliki.