Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Hakimiliki Tanzania

To protect the rights of content creators...
COSOTA KUTOA ELIMU KWA VIONGOZI WA CHAMUDATA NA WANACHAMA WAKE
21 Apr, 2023
COSOTA KUTOA ELIMU KWA VIONGOZI WA CHAMUDATA NA WANACHAMA WAKE

Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Doreen Anthony Sinare leo Aprili 12,2023 amefanya kikao na viongozi wa Chama cha Muziki wa Dansi nchini (CHAMUDATA).

Kikao hicho kililenga kujadili namna bora ya kutatua  changamoto za masuala ya hakimiliki kwa Wasanii wa Muziki wa dansi ili waweze kunufaika na kazi zao.

"Mwezi Mei, 2023 tutaandaa mafunzo kwa viongozi wa CHAMUDATA na baadae kwa Wanachama wote hii ni kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki na mikataba ili muweze kufuatilia haki zenu kwa mujibu wa Sheria," alisema Doreen.

Akizungumza katika kikao hicho Katibu Mkuu wa CHAMUDATA Said Kiberiti alieleza changamoto mbalimbali ambazo zinachangia kudidimiza mapato ya kazi za Wasanii wa  Muziki wa dansi kuwa moja wapo kuwa ni uharamia kwa njia ya mitandao, kukosekana kwa vipindi vya Muziki wa dansi katika vyombo vya habari pamoja na uelewa mdogo wa masuala ya hakimiliki.

Pamoja na hayo Kiberiti aliomba COSOTA kushirikiana na CHAMUDATA kufuatilia kazi za Wasanii wa Muziki wa Dansi walizorekodi na Redio Tanzania hapo zamani.

Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki huyo aliahidi kuwapa ushirikiano na kushauri uongozi huo kuwa wabunifu katika namna ya kuendesha shughuli zao ikiwemo kuweka mkakati wa viwango vya kufanya show katika maeneo ya burudani ili waweze kunufaika na pia kuangalia suala la nyimbo zinazorudiwa katika bendi na mbalimbali.