WAZIRI DKT. NDUMBARO ASISITIZA WABUNIFU KAZI ZA SANAA KUJISAJILI
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewasisitiza wasanii, wandishi wa vitabu na wabunifu kujisajili na kusajili kazi zao katika ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ili waweze kunufaika na kazi zao pamoja na fursa za mikopo zinazotolewa na taasisi za fedha.
Mhe. Ndumbaro amesema hayo tarehe 27, 2024 mjini Songea wakati akifungua
mafunzo ya urasimishaji wa kazi za sanaa, uandishi na ugawaji wa vitabu na vifaa vya majaribio vya kusaidia kusoma kwa shule zenye wanafunzi wenye uhitaji maalum.
Ametoa rai kwa wadau hao kujirasimisha na kurasimisha kazi zao ili zitambulike rasmi, huku akiwaagiza COSOTA na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania kuwafikia wadau hao hasa waliopo mikoa ya pembezoni ili waweze kuwa na uelewa na faida ya urasimishaji.
"Urasimishaji una faida nyingi ikiwemo usimamizi wa kazi zenu kwa ufanisi, kulindwa na sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki na fursa za biashara zaidi kwa kuwa mtakua mnatambulika, pia mtaweza kuongeza kipato binafsi na Taifa kwa ujumla na kupanua soko la kazi zenu", amesisitiza Mhe. Ndumbaro.
Ameongeza kuwa, Sekta ya Utamaduni na Sanaa inaongoza kwa ukuaji kwa asilimia 19, ambapo amesema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inaelekeza sekta hiyo kukua na kuajiri vijana wengi ambapo wizara inaendelea kutekeleza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Sanaa, Dkt. Emmanuel Ishengoma amesema
sekta ya ubunifu ina vipaji vingi ambavyo vinahitaji elimu ya kurasimisha kazi hiyo na wao kama wizara watahakikisha wanaendelea kutoa elimu ya urasimishaji.
Awali Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa HakiMiliki, Bi. Doreen Sinare amesema mafunzo hayo pia yameambatana na utoaji wa vifaa vya majaribio kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wenye uoni hafifu kwa baadhi ya shule za mkoa huo ambavyo vitawasaidia kuandaa rejea na masomo katika kuandaa vitini.
Mafunzo hayo yamejikita katika mada mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kujisajili BASATA, huduma zinazotolewa na Bodi ya Filamu, Hakimiliki na umuhimu wa usajili wa kazi za sanaa na uandishi pamoja na fursa za mitaji kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa.